Sunday, January 1, 2012

MPIGA PICHA MWANDAMIZI WA IDARA YA MAELEZO Z'BAR AFARIKI

Na Haroub Hussein.

WAANDISHI wa Habari wapiga picha wa Zanzibar na Tanzania kwa ujumla wameuanza mwaka 2012 katika hali ya huzuni baada ya Mpiga Picha Mwandamizi Mwinyimvua Ahmed Ali (56) kufariki Dunia leo mchana katika Hospitali ya Rufaa ya Mnazimmoja alipokua amelazwa tangu juzi katika wodi ya wagonjwa mahtuti akisumbuliwa na Shindikizo la damu.

Mwinyimvua ambaye alikua Mpiga picha wa Rais wa Zanzibar kwa muda wa miaka 20 akiwa mpiga picha wa Rais wa Awamu ya tano ya Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar Dk. Salmin Amour Juma sambamba na Rais wa awamu ya sita Dk. Amani Abeid Karume.

Kwa mujibu wa taarifa iliyotolewa na Idara ya Habari Maelezo Zanzibar , Mwinyimvua aliajiriwa na iliyokua  Idara ya Habari na Utangazaji akiwa na umri wa miaka 18 kama mpiga picha mwanafunzi.
Aidha marehemu alikwenda Nchini Japan kwa mafunzo ya mwaka mmoja ya upigaji picha, baada ya kurudi Zanzibar marehemu alihamishiwa katika ofisi ya Rais Ikulu akiwa Mpiga picha wa Rais.

Katika mwaka 2011 marehemu alihamishiwa Idara ya Habari Maelezo Zanzibar ambapo alikua mpiga picha Mwandamizi wa Idara hiyo.
Marehemu Mwinyimvua ameacha mke na watoto watano, anatarajiwa kuzikwa kesho saa saba mchana kijijini kwao Fuoni Wilaya ya Magharibi Unguja .

MUNGU AILAZE MAHALI PEMA PEPONI ROHO YA MAREHEMU.AMIN.

1 comment:

  1. Ingawa ni muda sasa lakini bado tunamkumbuka na kuthamini mchango wake kwani kuna mengi ya kujifunza katika utumishi wake kwa umma na utii kwa viongozi wake wa kazi.

    Bila shaka mungu atampa kila lenye kheri naye, aamin.

    ReplyDelete