Sunday, October 31, 2010

NA HAROUB HUSSEIN,ZANZIBAR.

ZEC  YAHAIRISHA UCHAGUZI WA WADI NNE ZA MJINI.
TUME ya Uchaguzi ya Zanzibar (ZEC) imehairisha Uchaguzi wa Wadi nne za Wilaya Mjini  katika Mkoa wa Mjini Magharibi kutokana na matatizo ya uchapishaji yaliyojitokeza katika karatasi za kupigia kura.
Akitangaza  hatua hiyo mbele ya Waandishi wa habari katika kituo kikuu cha kutangazia matokeo kilichopo katika ukumbi wa salama hoteli ya Bwawani Mkurugenzi wa ZEC,ndugu Salum Kassim Ali alisema tume imefikia uwamuzi huo baada ya mkutano wao ulioshirikisha uongozi wa Tume pamoja na kuwajuilisha wagombea wote wa Udiwani wa wadi husika.
Alisema wakati  Tume ikiendelea na usambazaji wa karatasi za kura katika vituo mbali mbali Unguja na Pemba ,Tume yake ilipokea taarifa kutoka kwa Msimamizi wa Uchaguzi wa Wilaya ya Mjini, juu ya mapungufu hayo.
Aidha alisema tatizo hilo limejitokeza katika wadi zilizomo katika majimbo manne,akiyataja majimbo yenyewe na wadi zenye zitakazohairishwa kuwa ni  Jimbo la Mji mkongwe  katika wadi ya mchangani. A mbapo wadi hiyo ilitakiwa kuwa na shehia ya Mchangani,Vikokotoni ,Mumbetanga na Malindi.Katika mapungufu yaliyojitokeza karatasi za Shehia ya Vikokoni zimechapishwa kwa wagombea wa wadi ya Mkunazini. 
Jimbo la Kwahani wadi itakayohairishwa kuwa ni  wadi ya kwahani.ambapo wadi hii ilitakiwa kuwa na shehia ya Kwahani,Kidongo chekundu na Kwaalamsha.katika mapungufu yaliyojitokeza katika uchapishaji kwenye karatasi za kupigia kura za Wadi hii ni kuwa karatasi za Shehia ya Kidongo chekundu zimechapishwa na karatasi za wagombea wa wadi ya Mikunguni.
Akiyataja majimbo men gine alisema Jimbo la Kikwajuni,katika wadi ya Miembeni ambapo wadi hii ilitakiwa kuwa na shehia ya Miembeni na Kilimani tatizo lililojitokeza ni kuwa karatasi za Shehia ya Kilimani zimechapishwa pamoja na karatasi za wagombea wa wadi ya Kikwajuni.
 Na Jimbo la Magomeni katika wadi ya Nyerere.ambapo wadi hiyo ilitakiwa kuwa na Shehia ya Sogea,Nyerere na Kwa wazee,tatizo lililojitokeza ni kuwa karatasi za kura za shehia ya Sogea zimechapishwa pamoja na karatasi za wagombea wa Nyerere.
Aidha alisema licha ya kuhairishwa na Uchaguzi  huo ,hakutakua na mabadiliko yoyote ya wagombea na hakutakua na muda mpya  wa kampeni.
“Licha ya Tume kuuhairisha Uchaguzi katika Wadi hizi hakutakua na mabadiliko yoyote ya wagombea na muda wa ziada wa kampeni.Vilevile kuahirika kwa Uchaguzi huu hakutaathiri Uchaguzi wa Raisi ,Wabunge na Wawakilishi katika majimbo husika”alisema mkurugenzi huyo.
Kassim alisema kutokana na mapungufu yaliojitokeza Tume imeamua  kuuhairisha Uchaguzi katika wadi hizo hadi tarehe 28 Novemba mwaka 2010.